Wednesday 16 December 2015

RAILA ODINGA MAGUFULI WA KENYA

Nasema bila woga wala shauku yeyote kwamba kenya yahitaji Magufuli wake. Tulionao kwa sasa sio Magufuli ila matatizo. Wakati ambapo Magufuli anafungua kufuli zote Tanzania uongozi wa Uhuru Kenyatta unaendeleza uhuru wa ufisadi Kenya. Sifa za Rais Magufuli na maamuzi yake ya kazi toka alipotwaa uongozi wa Tanzania zimewafikia hata wakenya. Wengi wamemsifia na wengine wameandika wakiomba Mungu awape Rais kama Magufuli. Kwa kipindi kifupi alichoingia madarakani, Rais Dkt. John Magufuli amefanya mambo kadhaa ambayo yamewaridhisha na kuwapa moyo Watanzania, mambo hayo ni kama, ziara yake ya kushtukiza kwenye hospitali ya Taifa la Muhimbili  iliyovumbua vitu vingi na kupelekea Rais Magufuli kufuta bodi ya Wakurugenzi wa hospitali hiyo pamoja na kumuondoa Kaimu Mkurugenzi wake, Kufuta safari za viongozi kwenda nchi za nje ili kupunguza matumizi makubwa ya pesa za Serikali, kuelekeza shilingi milion 225 zilizochangwa kwa ajili ya kugharamia hafla ya Pongezi za Wabunge Dodoma kutumika kununua vitanda vya hospitali na shilingi milion 15 tu ndio zitumike kwa ajili ya sherehe hiyo.  Jumatatu ya tarehe 23 November 2015, Rais Dkt. John Magufuli alitangaza kufuta kwa sikukuu ya Uhuru December 9 na kuagiza fedha za maandalizi ya sikukuu hiyo zitumike kutatua matatizo mengine pia ameagiza siku hiyo itumike kusafisha mazingira ili kupunguza matatizo ya kipindupindu nchini. Huyu ndiye Rais mtajika wa Tanzania ambaye huwezi mlinganisha na huyu wetu wa ziara na vihoja vya kila siku. Wetu ni ukatuni na wajali maslahi yao bila ya kujali taifa. Wetu wajifanya waumini ilhali ni mafisi. Hawa wetu hawawezi saidika hata na maombi kwani sikio la kufa halisikii dawa. Dawa ya hawa makabwela ni moja tu! Wakenya wakubali sura ya kutuongoza na nyuma ya hiyo sura kuwe na vijana chipukizi wana mabadiliko watakao kaa macho kwa kila maamuzi ya taifa hili. Je, sura ni nani? Sura ya Magufuli kenya ni Raila Odinga. Kenya sasa yahitaji RAILA AMOLO ODINGA kuchukua nafasi ya Urais na kuikomboa Kenya kutoka kwa vijana hawa wawili waliochanganyikiwa na uongozi kiasi ya kuacha taifa nzima uchi. Vijana waliojaa kasumba ya kula na kulala uchi. Vijana walio na damu moto sio ya kuendeleza nchi bali ya kubaka demokrasia ya wakenya na kenya kwa jumla. Hawa hawana doa la uongozi damuni mwao. Walicho nacho ni damu ya dhumla walioiridhi kutoka kwa watangulizi waliokuwa hapo awali. Wao ni KANU na KANU ni wao. Sera ni zile zile za kihayawani, hamna kujali raia wake. Kwao wao raia ni ufisadi kila siku. Enyi wakenya wapenda amani someni historia ya taifa hili. Waskizeni wazee na mjaribu kufungua macho muone kila kitu kwa jicho la tatu wala sio jicho la ukabila. Nani asiyejua kwamba historia ya Kenya haiwezi andikwa sahihi bila kuwepo mchango wa Raila Amollo Odinga? Uhuru Kenyatta na William Ruto hawapo kwenye historia ya kenya. Mmoja ni mtoto wa hayati Mzee Jomo Kenyatta na mmoja ni mtoto wa Daniel Toroitich Arap Moi. Kwa ufupi wote ni watoto wa KANU. Hawajui shida wala njaa, wote walipakuliwa pilau pasi na kujua chakula hiyo inatoka wapi. Kama ni historia basi kwa hawa wawili ni historia ya dhulma na ufisadi wa hali ya juu. Fikra za wawili hawa hazibadiliki, uzembe, unafiki wa hali ya juu, ufisadi na ufujaji wa mali ya umma ni jambo la kawaida kwao. Uhuru Kenyatta ni Rais asiyetulia, utadhani yeye ni waziri wa mambo ya nje na wala sio Rais naye William Ruto utadhani ni mlinzi wa Rais kwani kila mara yumo nyuma yake. Ziara yake huko Paris, Ufaransa na ‘waziri wake mpya wa mazingira’ (Ngina Kenyatta) siku moja tu baada ya kuondoka kwa Papa Francis kunaonyesha wazi kuwa Rais hajali jinsi anavyotumia pesa za wakenya. Sasa ziara za serikali zinahusisha watoto wake ambao utadhani ni mawaziri wa humu nchini. Hii ni dalili ya uongozi duni usio na mbele wala nyuma. Someni historia jameni! Na ndio maana ningelipenda kutaja kwamba historia itakapoandikwa kuhusu  maendeleo na upanuzi wa demokrasia nchini Kenya, Raila Amollo Odinga atatengewa  sura nyingi. Sura za shujaa na mpenda kenya aliye na utaifa ndani yake. Kiongozi aliyepigana vita mamluki na wafisadi wakubwa nchini. Rais wa watu aliyedhulumiwa katika chaguzi mbili. Huyu ndiye Magufuli wa Kenya mwaka wa 2017. Hulka yake ni kubainisha mbivu na mbichi. ukweli huu umedhihirika wazi tunaposoma  historia kuhusu waanzilishi wa taifa hili waliojitahidi sana kuikomboa Kenya kutoka utawala dhalimu wa wakoloni.  Historia huzama zaidi za kuonyesha mchango wa kila mmoja kwa namna inayotuchorea taswira  ya mwono-ulimwengu wa kila mmoja. Lakini kwa kuwa historia ni tundu, inafumbata mambo haya kwa uketo wa kuajabisha sana. Je, ni funzo gani ambalo Raila Odinga anapaswa kupata kutokana na misukosuko ya mawimbi ya siasa ambayo amepitia katika kipindi chake kirefu cha miongo kadha ya siasa za ukombozi? Raila Odinga sasa anafaa alegeze kamba na kuwakubali vijana kuingia ndani ya chama chake na kuongeza nguvu ya kupambana na hawa mafisadi wakubwa. Raila ni sharti akubali kushirikiana na vijana, awape nafasi, mawaidha kisha akae kando aone vile ambavyo vijana hao watakomboa kura zake zote. Bila ya vijana Raila haendi popote. Wanaomzingira Raila wafaa wamweleze haya bila woga, wamweleze afungue mlango wake wazi na aache vijana wanaotaka kumsaidia kuchukua uongozi kufanya hivyo ki-demokrasia bila ya wao kunyimwa nafasi za kufanya hivyo. Hii ndio silaha ya mwisho ya Raila Amollo Odinga. Raila ni jabali ambaye sasa anahitaji vijana kufanikisha ndoto yake ya kuwakomboa wakenya. Jina la Raila haliuziki ila lafahamika na kila mkenya. Sifa zake zinazidi kubobea kila kukicha. Anachohitaji sasa ni kuongeza makali na damu mpya ndani ya chama chake. Damu moto ya vijana wanaotaka mabadiliko kwa mpigo mmoja tu. Punda amechoka na vijana pia wamechoka! Ifahamike wazi kuwa mtu huzaa neno. Neno hilo likawa kubwa kumzidi mtu huyo aliyelizaa na hatimaye likambwaga. Ninaamini kwamba siku moja, ndoto za Raila Odinga  hazitakuwa ni ndoto tu – bali ukweli mtupu. Ukweli ambao labda wengi wanaogopa kuusema ni kwamba demokrasia ya Kenya itamaskinika bila Raila Odinga kushika usukani wa kisiasa nchini Kenya. Wasemavyo waswahili heri kafiri akufaae kuliko silamu asiyekufaa na zimwi likujualo halikuli likakumaliza. Ya Uhuru Kenyatta na William Ruto tumeona na hatutaki kusikia tena. Kelele zao za kusema na kutenda na waziseme wakiwa nje ya ikulu mwaka wa 2017. Historia itajiandika tena mwaka wa 2017. Kenya yahitaji Magufuli wake wa tangu na mwaka wa 2007 na 2013. Magufuli wa Kenya Raila Odinga. Kwa viongozi mnaoongoza kwa misingi ya kikabila jueni zenu zimefikia kikomo. Narudia tena, enyi wakabila wakubwa mnaoongoza kwa ukabila kumbukeni Raila hakuwa mwendawazimu aliposema Kibaki Tosha licha ya kujua fika Mwai Kibaki ni mkikuyu na pili kujua alivyofanywa babake Jaramogi Oginga Odinga miaka ya nyuma yote aliyatupa katika kaburi la sahau na akatizama taifa na utaifa. Je, hapakuwa na makabila mengine? Je, mkikuyu na Mkalenjin mgani leo yupo tayari kusema Raila tosha? Kama yupo jawabu asinipe lakini alitoe 2017.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Kuwasiliana naye: mali@standardmedia.co.ke, FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Twitter: @mohajichopevu